SERIKALI imesema shule zote zenye nafasi
za wanafunzi wa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu, zimejaa hivyo
hakuna nafasi ya mwanafunzi kubadilishiwa shule au mchepuo aliochagua.
Hayo yalibanishwa jana katika taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya
habari mjini hapa na Msemaji wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi), Rebecca Kwandu.
Kwandu alisema baada ya serikali kutangaza wanafunzi waliojiunga na
kidato cha tano, baadhi ya wazazi na wanafunzi wamekuwa wakifika ofisi
za Tamisemi kuomba kubadilishiwa shule au tahasusi (michepuo)
walizochaguliwa.
“Tunapenda kuwaarifu kwamba shule zote zenye nafasi za wanafunzi wa
kujiunga na kidato cha tano mwaka 2016 zimejaza, hivyo hakuna
kinachoweza kubadilishwa,” alisema Kwandu.
Aidha, Kwandu alisema vigezo ambavyo vilitumika katika uchaguzi huo ni
pamoja na ufaulu na uchaguzi wa wanafunzi wenyewe juu ya masomo
wanayopenda kuendelea nayo kidato cha tano na sita.
“Kulingana na utaratibu uliowekwa na serikali, mwanafunzi mwenye sifa
za kuchaguliwa kuendelea kidato cha tano na vyuo vya ufundi ni yule
ambaye ufaulu wake ni kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu. Wanafunzi
hao wamepangwa kulingana na ufaulu wao masomo waliyochagua na nafasi
zilizopo,” alisisitiza.
Pia alisema nafasi za shule walizopangiwa wanafunzi zimezingatia
miundombinu ya shule husika na uwezo, na kwamba kila shule imepewa
wanafunzi kulingana na nafasi zilizopo, hivyo hakutakuwa na nafasi ya
kuwabadilisha kutoka shule moja kwenda nyingine kwa sasa.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga
na kidato cha tano na vyuo vya ufundi kuripoti katika shule na vyuo
walivyopangiwa kama walivyoelekezwa.
Alisema mwanafunzi ambaye hataripoti ifikapo Julai 24, ambayo ni tarehe
ya mwisho kwa muda uliopangwa, atakuwa amepoteza nafasi yake kwa kuwa
itachukuliwa na mwanafunzi mwingine ambaye hakupata nafasi awali.





0 Comments