Inasemekana kwamba haijalishi kama mume/mwenza wako ni pacha ama ametoka
kwenye familia yenye historia ya mapacha. Mwenye uwezo wa kusababisha
watoto mapacha ni mwanamke pekee. Ikiwa na maana mwanamke ambaye ni
pacha ama ndugu zake wa kike kama vile dada, mama wana historia ya kuwa
na mapacha ama wao ni pacha basi mwanamke huyo ana nafasi kubwa ya
kupata watoto mapacha.
Kwa mfano: Mwanamke ambaye mke wa mjomba wake ana mapacha haimpi yeye
nafasi ya kupata mapacha kwa sababu hana uhusiano na mke wa mjomba wake
kibailojia. Ila mwanamke ambaye dada yake ana mapacha inampa uwezekano
wa kupata watoto mapacha kwasababu wana uhusiano wa moja kwa moja.
Hembu tujifunze hatua moja baada ya nyingine. Kwanza tufahamu mimba
inatungwa vipi? Na kisha tuone jinsi gani mimba ya watoto mapacha
inavyotungwa.
Mimba inatungwaje?
Kipindi cha ovulation ndipo ambapo mwanamke anaweza kushika mimba.
Ovulation ni kipindi ambacho yai kubwa ama yai lililo tayari hutoka
kuelekea kwenye tumbo la uzazi kupitia mirija ya ovari. Yai hilo kwa
bahati nzuri likikutana na mbegu ya kiume hurutubishwa katika kipindi
cha masaa 24 (baada ya muda huo yai hupoteza uwezo wake). Iwapo yai
litarutubishwa ndani ya muda huo na kisha kujikita katika mfuko wa uzazi
basi mimba itakuwa imetungwa. Iwapo yai halikurutubishwa hutolewa nje
kama damu ya hedhi.
Mapacha hutokeaje?
Hapa tukumbuke kuwa kuna mapacha wa aina mbili: Mapacha wanaofanana
(Identical twins) na Mapacha wasiofanana (Fraternal twins). Mapacha
wasiofanana hutokea pale mwanamke anapotoa mayai mawili kuelekea kwenye
tumbo la uzazi. Hii ina maana ni mwanamke ama mwili wa mwanamke
unaosababisha mayai mawili kuachiliwa kwa pamoja. Baada ya hapo mayai
haya hukutana na mbegu za kiume ambapo hurutubishwa ndani ya muda
maalumu na kisha hujikita kwenye mfuko wa uzazi. Hivyo basi hata kama
mwanaume angetoa mbegu milioni moja lakini yai la mwanamke likitoka moja
basi mtoto atakayepatikana atakuwa ni mmoja tu.
Huo ni upande wa mapacha wasiofanana (Fraternal twins). Kwa upande wa
mapacha wanaofanana (Identical twins) hadithi ni tofauti kidogo. Baada
ya yai kurutubishwa na mbegu ya kiume na kujikita kwenye mfuko wa uzazi
kwa sababu zisizofahamika kisayansi huamua kujigawa na kutengeneza
watoto mapacha. Mapacha hawa kwa kawaida hufanana sana na huwa ni wa
jinsia moja tofauti na fraternal twins ambao huweza kuwa wa jinsia mbili
tofauti ama jinsia moja.
Kutokana na maelezo hayo hapo juu inaonyesha kwamba watoto mapacha
wanaofanana ama wasiofanana husababisha na mwanamke ambaye kwa sababu
moja ama nyingine mwili wake huachilia mayai mawili ama hugawanya yai
lake lililorutubishwa na kusababisha watoto mapacha. Japokuwa kumekuwa
na mabishano makali ambapo watu wengine wamekuwa na maoni hususani kwa
upande wa mapacha wanaofanana kwa kusema kwamba mbegu ya kiume huwa na
nguvu zaidi na hivyo kugawanya yai. Sina uhakika na jambo hilo ila kwa
tafiti nyingi zilizofanywa na wanasayansi zinasema mwanamke ndiye mwenye
uwezo wa kusababisha watoto mapacha yeye ama ndugu zake wa kike
(wanaohusiana kibaiolojia).
Sababu nyingine zinazoweza kuchangia watoto mapacha
1. Mwanamke anayetoka kwenye familia ambayo wanawake wana historia ya kupata mapacha.
2. Wanawake wenye asili ya kiafrika na kimarekani.
3. Wanawake wanaobeba mimba wakiwa na umri mkubwa, kuanzia miaka 35.
4. Wanawake wanene na wale warefu.
Hitimisho
CHANZO:Udakuspecially
0 Comments